CHANJO KWA WATOTO WENYE UMRI CHINI YA MIAKA MITANO
- Mwili wa binadamu unauwezo wa kupambana na magonjwa mbalimbali lakini huitaji kinga imara ili uweze kupambana na hayo magonjwa, kinga dhidi ya magonjwa hutengenezwa na mwili pale tu mwili unapopata maambukizi ya ugonjwa husika kwa mara ya kwanza, hivyo basi mwili hauwezi kuwa na kinga mathubuti ya ugonjwa husika kama haujapata maambukizi ya huo ugonjwa kwa mara ya kwanza.
- Hii inamaanisha mwili unahitaji maambukizi ili uwe na uwezo wa kupambana na magonjwa, hii ilipelekea wanasayansi kuvumbua kitu kinaitwa chanjo. Chanjo ni kitu kilichotengenezwa maabara na wanasayansi kwaajiri ya kuuchochea mwili kutoa au kutengeneza kinga mathubuti dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuirika.
- Mtoto mchanga anapozaliwa mwili wake hauna kinga imara zakuweza kupambana na kujikinga na magonjwa mbalimbali, kwa wakati huo mwili wa mtoto hutumia kinga ya kurithi kutoka kwa mama yake mzazi, ambapo kinga hii huwa sio imara sana kwa magonjwa mbalimbali. Kadri mtoto anavyozidi kukua na kupata maambukizi ndipo mwili wake unatengeneza kinga, kwa wakati huo mtoto huitaji chanjo na lishe bora ili mwili wake uweze kutengeneza kinga imara dhidi ya magonjwa mbalimbali.
- Chanjo za watoto chini ya miaka mitano hutengenezwa maabara za kisayansi kwa ufanisi mkubwa na kabla hazijatumika kwa binadamu hujaribiwa kwa wanyama ili kuona kama zina sababisha madhara yoyote yale, hivyo kuzifanya salama kwa matumizi ya binadamu.
- Chanjo hizi hazina madhara ya kiafya kwa binadamu lakini matumizi yake huambatana na maudhi madogo madogo kama vile homa na maumivu. Chanjo hizo hupatikana kwenye vituo vya afya bure, na hutolewa kwa njia mbalimbali lakini nyingi hutolewa kwa njia ya sindano na matone kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Zifuatazo ni aina ya chanjo mbalimbali zinazotolewa na kupatikana nchini tanzania.
- BCG; hii ni chanjo inayotolewa kwa mtoto mchanga mara baada ya kuzaliwa au ndani ya miezi mitatu, huchomwa kwenye bega la kulia na huacha alama ya kovu (ndui), chanjo hii hutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu. Kama mtoto atachomwa hii chanjo na kovu lisitoke, mtoto huyo hutakiwa kurudia tena.
- POLIO; hii chanjo hutolewa katika nyakati tofauti, polio zero hutolewa mara baada ya mtoto kuzaliwa, na zingine huendelea mara baada ya mtoto kufikisha wiki sita. hii chanjo ipo kwenye hali ya maji na hutolewa kwa njia ya matone, chanjo hii hutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa kupoonza mwili. Hakikisha mtoto wako anapata chanjo hii mara nne.
- PCV; hii ni chanjo inayotolewa kwa watoto waliofikisha wiki sita sawa na mwezi mmoja na nusu, chanjo hii hutolewa mara tatu kwa njia ya sindano kuanzia wiki ya 6, 10 na 14, ambapo mtoto huchomwa kwenye paja la kulia, chanjo hii hutoa kinga dhidi ya maambukizi ya homa ya mapafu kwa watoto. Hakikisha mtoto wako anachomwa chanjo hii mara tatu.
- DPT-HbB; hii chanjo hutolewa kwa watoto waliofikisha wiki sita baada ya kuzaliwa, chanjo hii hutolewa kwa njia ya sindano, ambapo mtoto huchomwa kwenye paja la kushoto mara tatu kuanzia wiki ya 6, 10, na 14. chanjo hii hutoa kinga dhidi ya magonjwa matano; kifaduro, donda koo, pepopunda, homa ya ini, na homa ya mafua. Hakikisha mtoto wako anapata chanjo hii mara tatu.
- MEASLES, MUMPS&RUBELLA; chanjo hii hutolewa mara mbili kwa watoto wenye umri wa miezi 9 na 18, hotolewa kwa njia ya sindano kwenye bega la kushoto, chanjo hii hutoa kinga dhidi ya maambukizi ya surua, matumbwitumbwi, na surua ya kijerumani. Hakikisha mtoto wako anapata chanjo hii mara mbili.
- ROTTA; chanjo hii hutolewa mara m,bili kwa watoto wenye wiki 6, na 10. hii chanjo ipo katika hali ya maji na hupewa mtoto kwa njia ya matone mdomoni. hii chanjo hutoa kinga dhidi ya maambukizi ya tumbo yanayosababisha kuharisha. Hakikisha mtoto wako anapata chanjo hii mara mbili.
No comments