MUDA MUAFAKA WA KUANZA KLINIKI YA MAMA-MJAMZITO.
- Mwanamke anapopatwa na ujauzito huwa na mawazo ni lini haswa anatakiwa aanze kuhudhuria kliniki ya afya ya uzazi haswa kliniki ya mama mjamzito, wengi wao hawafahamu ni lini muda muafaka wa kuanza kuhudhuria kliniki hali ambayo huwafanya wachelewe kupata huduma sitahiki ya mama mjamzito.
- Mama-mjamzito anatakiwa kuanza kliniki ya afya ya uzazi pale tu anapogundulika kuwa ni mjamzito, kuwahi kuanza kliniki humsaidia mama-mjamzito kupata huduma stahiki mapema zinazoendana na umri wa mimba, hivyo hivyo mama mjamzito anapochelewa kuanza kliniki kwa wakati husababisha kukosa baadhi ya huduma zinazoendana na umri wa ujauzito.
- Kliniki ya afya ya uzazi si kliniki ya wajawazito tu, hata akina baba inawahusu na inashauriwa mama-mjamzito anapoanza hii kliniki aende na mume/mwenzi wake. Mama mjamzito akianza kliniki hupangiwa mahudhurio yake kutokana na afya yake na afya ya ujauzito wake, katika kipindi hiki mama mjamzito anatakiwa kuonana na watoa huduma wa afya si chini ya mahudhurio nane.
HUDUMA ZINAZOPATIKANA KLINIKI YA AFYA YA UZAZI/WAJAWAZITO.
Katika mahudhurio yote atakayohudhuria mama-mjamzito na mwenzi wake anatakiwa ahakikishe anapata huduma zifuatazo.
- Kadi ya kliniki; mama-mjamzito lazima apatiwe kadi ya kliniki katika hudhurio lake la kwanza na kadi hiyo lazima ionyeshe tarehe yake ta makadilio, umri wa mimba, na vitu vingine vinavyomhusu mama na mtoto.
- Vipimo vya magonjwa; mama-mjamzito na mwenzi wake wanatakiwa wafanyiwe vipimo hasa kwenye hudhurio la kwanza, vipimo vya magonjwa yanayoambukizwa kama vile UKIMWI, kaswende, kisonono, na vipimo ya magonjwa yasioambukizwa kama vile msukumo wa damu, kisukari na magonjwa ya moyo.
- Chanjo; mama mjamzito anatakiwa apewe chanjo ya pepopunda, ambayo humkinga yeye na mtoto wake.
- Tiba kinga; mama-mjamzito kutokana na umri wa ujauzito wake anatakiwa apewe kinga za magonjwa mbalimbali anayoweza kuyapata katika kipindi cha ujauzito na kuhatarisha afya ya ujauzito, hivyo basi mama-mjamzito hupewa kinga dhidi ya malaria, na minyoo.
- Lishe mbadala; katika hudhurio la kwanza mama-mjamzito hupewa dawa za kuongeza damu, vitamins, na madini ya mwili kama lishe mbadala, dawa hizi humsaidia mtoto katika ukuaji na maendeleo yake.
- Maendeleo ya mtoto; katika kila hudhurio, mama-mjamzito hupimwa ukuaji na maendeleo ya mtoto, pia katika kila hudhurio mama-mjamzito anatakiwa ajue umri wa mimba kwa wiki, mapingo ya moyo ya mtoto, mlalo wa mtoto, na kitangulizi cha mtoto.
- Vipimo vya mwili; katika kila hudhurio mama-mjamzito anatakiwa apimwe uzito na urefu wake.
No comments